Rodri ashinda tuzo ya Ballon d’Or 2024
Kiungo wa kati wa Klabu ya Manchester City na Hispania Rodri ameshinda tuzo ya Ballon d’Or kwa wanaume – tuzo ya mwanasoka bora wa mwaka 2024 – kwa mara ya kwanza.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28, ambaye alipoteza mchezo mmoja pekee msimu uliopita kwa klabu na taifa, alitwaa tuzo hiyo huko Paris baada ya kuisaidia Uhispania kushinda Euro 2024 mwezi July 2024.
Pia Rodri alishinda Ligi Kuu ya England, UEFA Super Cup na Klabu Bingwa ya Dunia akiwa na Manchester City.
Rodri, amekuwa mchezaji wa kwanza katika historia ya klabu ya Manchester City kushinda Ballon d’Or, akishinda tuzo hiyo mbele ya winga wa Real Madrid na Brazil Vinicius Jr.
Kiungo wa kati wa Real Madrid, Jude Bellingham alikuwa wa tatu, akiwa mchezaji wa juu zaidi wa Uingereza aliyemaliza katika tuzo hiyo tangu Frank Lampard kumaliza katika nafasi ya pili mwaka 2005.
Real Madrid ilishinda tuzo ya klabu bora ya mwaka na meneja wao Carlo Ancelotti alikuwa mshindi wa tuzo ya kocha bora wa mwaka wa wanaume, lakini hakukuwa na mtu yeyote kutoka klabu aliyehudhuria kwaajili ya kupokea zawadi hizo.
“Siku maalum kwangu, familia yangu na nchi yangu,” alisema Rodri, ambaye alionekana jukwaani akitembea kwa magongo baada ya kupasuka kwa mishipa yake ya mbele ya mguu (ACL) mwezi September 2024.
“Leo sio ushindi kwangu, ni kwa mpira wa miguu wa Uhispania, kwa wachezaji wengi ambao hawajashinda na wamestahili, kama [Andres] Iniesta, Xavi [Hernandez], Iker [Casillas], Sergio Busquets, wengi sana.. Ni kwaajili ya soka la Uhispania na sura ya kiungo cha kati.”
Tuzo ya Ballon d’Or inamtambua mwanasoka bora wa mwaka na hupigiwa kura na baraza la waandishi wa habari kutoka kila moja ya nchi 100 bora katika viwango vya ubora vya Fifa duniani kwa wanaume.
Ilikuwa ni mara ya kwanza tangu 2003 ambapo mshindi mara nane Lionel Messi au mshindi mara tano Cristiano Ronaldo hawakuonekana kwenye orodha ya walioteuliwa.
Akiwa ameisaidia Manchester City kutwaa Treble {Mataji Matatu} mwaka 2023, Rodri alimaliza wa tano katika tuzo ya Ballon d’Or mwaka jana 2023.
Mafanikio yake yanayoendelea akiwa na Manchester City na nafasi yake ndani ya timu ya Uhispania iliyoshinda Euro 2024 imemfanya kuwa mmoja wa wachezaji wenye ushawishi mkubwa katika soka la Dunia.
Mchezaji huyo wa kati alitoka nje akiwa ameumia wakati wa mapumziko katika mechi ya Fainali ya Euro dhidi ya Uingereza, lakini alikuwa tayari amefanya ya kutosha kutangazwa mchezaji bora wa michuano hiyo.
Rodri alifunga mabao tisa bora zaidi kwa Manchester City msimu uliopita, ikijumuisha magoli mawili muhimu ya dakika za mwisho katika mechi za Ligi Kuu ya Uingereza na bao katika ushindi wa 3-1 dhidi ya West Ham United.
“Leo marafiki wengi wameniandikia na kuniambia kuwa soka imeshinda, kwa kuwapa nafasi viungo wengi wa kati ambao wana kazi nyingi na leo inadhihirika,” aliongeza Rodri ambaye alikabidhiwa tuzo hiyo mwaka na mshindi wa mwaka 1995 George Weah.
“Mimi ni kijana wa kawaida mwenye maadili, ambaye anasoma, ambaye anajaribu kufanya mambo sawa , na nimeweza kufika kileleni na ni shukrani kwenu nyote. ”
Alipoulizwa kuhusu jeraha la ACL ambalo litamfanya awe nje kwa msimu huu, alisema: “Ninajaribu tu kujitunza, kupumzika, kufurahia wakati wa mapumziko na familia yangu na nirudi nikiwa na nguvu zaidi.”
Kwa upande wa Harry Kane na Kylian Mbappe wao walishiriki Tuzo ya Gerd Muller – tuzo ya mfungaji bora – baada ya wote kufunga mabao 52 katika mashindano yote msimu uliopita.
Huku Mshambuliaji wa Real Madrid na Ufaransa Kylian Mbappe akiwa hayupo, nahodha wa Uingereza Kane alikabidhiwa tuzo hiyo kufuatia msimu mzuri wa kwanza akiwa na Bayern Munich.
“Asante kwa klabu yangu ya Bayern Munich, wafanyakazi wangu wote, wachezaji wenzangu, kwa kunisaidia kufunga mabao yote niliyofunga,” alisema Kane, ambaye alimaliza katika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa tuzo ya Ballon d’Or kwa wanaume.
“Ni heshima kuchukua tuzo hii kutoka kwa gwiji wa klabu [Karl-Heinz Rummenigge] – asante sana.”
0 Comments
Post a Comment