MGOMBEA mwenza wa kiti cha urais wa Chama Cha Mapinduzi, Dk. Emmanuel Nchimbi, ameahidi iwapo chama hicho kitapewa dhamana ya kuongoza nchini, kitakamilisha ujenzi wa Hifadhi ya Viwanda vya Usindikaji wa Kilimo na Maziwa katika Jimbo la Kwela, Wilaya ya Sumbawanga, mkoani Rukwa, ndani ya kipindi chake cha miaka mitano.
Dk Nchimbi ametoa kauli hiyo leo Septemba 8, 2025 alipowasili mjini Sumbawanga kwa ajili ya mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Laela. Alitumia nafasi hiyo kukuza sera za chama na kuwaunga mkono wagombea wa CCM katika ngazi ya udiwani, ubunge na urais.
Alieleza kuwa, pamoja na Hifadhi ya viwanda, Serikali ya CCM ina mpango wa kujenga vituo vitatu vipya vya afya katika Wilaya ya Sumbawanga - kimojawapo kitakuwa katika Kata ya Laela, Jimbo la Kwela, kulikofanyika mkutano huo.
Dk Nchimbi pia alitangaza mpango wa ujenzi wa madarasa mapya 203 kwa shule za msingi na vyumba 250 kwa shule za sekondari za Kwela.
Aidha, alisema kuwa soko kubwa la kilimo litajengwa Laela ndani ya Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga.
Katika sekta ya maji, Dk.Nchimbi aliangazia mipango ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama kwa kujenga mabwawa ya maji na kuchimba visima virefu vya ziada. Alisema lengo ni kuhakikisha watu wasiopungua 90 kati ya 100 wanapata maji safi na salama ya kunywa.

0 Comments